Jumanne 27 Oktoba 2026 - 20:00
Sheikh Adel Sha’la Aonya Ukiukwaji Mkubwa wa Haki za Wafungwa Bahrain

Hawza/ Sheikh Adel Sha’la, mmoja wa wanazuoni wa Kishia nchini Bahrain, amekosoa vikali sera za mamlaka zinazotawala nchini humo, huku akionya kwamba utawala na uingiliaji katika masuala ya dini, ukosefu wa uhuru wa mahakama na kuendelea kukiukwa haki za wafungwa vimehatarisha njia ya kufikia haki nchini humo.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Adel Sha’la, mmoja wa wanazuoni wa Kishia nchini Bahrain, amezikosoa sera za mamlaka zinazotawala nchini humo na kuonya kuhusu kuingiliwa masuala ya dini, ukosefu wa uhuru wa mfumo wa mahakama na kuendelea kukiukwa haki za wafungwa.

Sheikh Adel Sha’la, akizungumzia uingiliaji wa mamlaka za utawala katika hukumu za Mwenyezi Mungu, alisisitiza kwamba; ni lazima kuchukua msimamo wa kisheria ulio wazi kuhusu maamuzi yanayohusiana na masuala ya dini, bila kuathiriwa na hesabu za kisiasa au maslahi binafsi.

Akieleza kwamba masuala hayo yanajumuisha kusimamisha swala, mambo ya wakfu, mirathi, malipo ya haki na mali, kutoa mwito wa kumwelekea Mwenyezi Mungu, pamoja na malezi na elimu ya kidini, aliwataka wanazuoni na waumini kutathmini kwa makini hali halisi iliyopo na kuweka wazi misimamo yao kuhusu yanayoendelea kutokea.

Alionya kwamba kuyachukulia masuala hayo kana kwamba yanawahusu watu wengine pekee hakumwondolei mtu wajibu wake wa kisheria.

Akiendelea, mwanazuoni huyo wa Kishia kutoka Bahrain alikosoa ukosefu wa uhuru wa mahakama na kubainisha kwamba; kufunguliwa kesi dhidi ya wanazuoni wa dini kumeibua wasiwasi mkubwa kuhusu uhakikisho wa kufanyika kesi za haki. Alitaka kuwepo mfumo huru wa mahakama ambao maamuzi yake hayaingiliwi na siasa, na ambao una dhamana zinazohitajika kulinda haki za washtakiwa.

Baadaye, Sheikh Adel Sha’la alizungumzia hali ya magereza na kunukuu kauli ya Amirul-Muuminina Imam Ali (a.s.), anayosema:

«السجن أحد القبرين»

“Gereza ni mojawapo ya makaburi mawili.”

Alieleza kwamba taarifa zinazotoka ndani ya magereza zinaonesha mateso na dhiki wanazopitia wafungwa, na kwamba maumivu hayo yamewakumba pia mama zao na familia zao.

Akikosoa mamlaka zinazotegemea nguvu na uungwaji mkono wa kikanda na kimataifa, wakati madai ya kutaka haki itekelezwe na haki za watu zilindwe yakiendelea, alionya kuhusu matokeo ya dhuluma. Katika suala hilo, alinukuu aya tukufu ya Qur’ani isemayo:

«وَسَيَعْلَمُ الَّذِينَ ظَلَمُوا أَيَّ مُنْقَلَبٍ يَنْقَلِبُونَ»

“Na wale waliodhulumu watakuja kujua ni marejeo gani watakayorejea.”
(Surat Ash-Shu‘ara, 26:227).

Mwisho, aliwataka wanazuoni na waumini ambao hawaoni hatari yoyote katika masuala ya dini wafikirie upya misimamo yao na kutathmini hali halisi kwa kuzingatia mambo yalivyo, bila upendeleo, alisisitiza kwamba msimamo wa kisheria unapaswa kuwa huru dhidi ya matamanio ya nafsi na maslahi ya kisiasa.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha